Friday, October 1, 2010

HUDUMA YA ELIMU, AFYA KUTOLEWA BURE INAWEZEKANA

Watanzania tusidanganyike kuambiwa kupata huduma ya afya na elimu haiwezekani!
Watu wengi wanaotafuta nafasi mbalimbali kutuongoza katika taifa letu la Tanzania wanatuambia kuwa huduma hizo zinaweza kutolewa bure.
Watu wengine wanapinga sana hoja hizo. Mimi nasikitika kuona kuna watu wanapinga wakisema huduma hizo haziwezi kutolewa bure!
Kadri yangu mimi nahisi inawezekana.
Kwanza, wakati wa mwalimu Nyerere miaka hiyo vitu hivyo vilitolewa bure kabisa. Kama katika kipindi hicho mambo hayo yaliwezekana iweje leo isiwezekane. Watuambia kitu ambacho kinafanya huduma hizo ziweze kutolewa bure.
Pili, wakati wa mwalimu Nyerere hapakuwa na miradi mingi kiasi cha miradi iliyopo sasa. Kadri ya wenyewe wanasema uchumi umekua. Kama uchumi umekua ina maana sasa tunao uwezo zaidi kuliko wakati huo. Kama tunao uwezo wa kiuchumi zaidi kuliko wakati huo, basi tunao uwezo zaidi wa kutoa huduma bure kuliko wakati ule.
Tatu, ufisadi mkubwa uliotokea katika nchi yetu unaashiria kwamba mali nyingi sana za nchi yetu zimefanya watu wengi tuamini kuwa kama pangekuwa na uaminifu katika serikali na ulinzi mahsusi wa mali za umma, basi watanzania wengi wangeamini kuwa huduma nyingi zaidi zenyi ubora zaidi zingewafikia Watanzania wengi zaidi.
Nne, misamaha ya kodi kwa wafanya biashara wakubwa inaonesha kuwa serikali haikusanyi mapato kwa makini zaidi ili kuhakikisha ina boresha huduma za jamii na pengine kuleta uwezekano wa kutoA HUDUMA HIZO BURE!
Tano, uzembe katika uimarishaji wa miundo mbinu yetu kwa ajili ya kukuza biashara zetu na nchi jirani unafanya watu waone kutoa huduma hizi bure haziwezekni! Kama tungeimarisha biashara yetu ya nje pato letu la taifa lingeongezeka sana na hivyo kuifanya serikali yetu iwe na uwezo wa kutoa huduma za kijamii bure.
Ukiangalia kwa makini sana utaona kuwa kutokuweza kufanya hivyo kunategemea sana watendaji wa serikali yetu waliopo madarakani. Kama wangejitoa kwa moyo wote kuwatumia wananchi mambo hayo yangewezekana.
Ili kuhakikisha tunakuwa na uwezo wa kupata huduma hizo za msingi bure, hatuna budi tudhamirie kweli tarehe 31-10-2010 tukapige kura na kuchagua viongozi wenye uwezo na mwelekeo chanya wa kuwatumikia wananchi kwa kuachana na viongozi mafisadi, wasio na uwezo wa kuona mbali na wenye ubinafsi ili wote na vizazi vyetu baadaye tufaidi matunda ya nchi yetu.

No comments: