Friday, September 24, 2010

HIVI NCHI YETU NI KILEMA!

Wakati akipiga kampeni jana, mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha mapinduzi, Mheshimiwa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alipigiwa simu na balozi wa Marekani hapa Tanzania. Baada ya kumaliza kuongea na huyo balozi, Mheshimiwa rais aliwaambia wananchi waliokuwa wanamsikiliza kuwa kupitia kwa balozi Obama, rais wa Marekani ameahidi kuendelea kutoa misaada Tanzania kwa sababu Tanzania inazingatia misingi ya uongozi bora.
 Kwa kweli mimi sikutegemea kabisa!
 Ndugu zanguni Watanzania, hivi nchi yetu ni kilema kweli kiasi cha hata rais wa nchi kuchekelea hawa mabepari wakubwa wanapoahidi kutoa misaada?
 Naomba sana tukumbuke kuwa Wazungu huwa hawatoi chochote pasipo faida kwao. Wazungu hawa ni wajanja wa muda mrefu sana. Kila wanachofanya kwetu sisi Waafrika, hukifanya kama mtego wa kutunasa wachukue kila kitu ambacho kina faida kwao.
 Wazungu hawa walianza kutuibia zamani sana. Hawa huiba vitu vingi kwa ujanja sana. Miaka ya zamani sana walitufanya sisi wanyama wakawa wanatuunza. Wametunyonya kama watumwa kwa miaka.Walipoona biashara ya utumwa haina faida kama mwanzo, wakatutawala kama wakoloni.
 Ukoloni huo umekwenda kwa miaka mingi tukinyonywa katika mambo mengi sana. Walitufanyisha kazi mashambani mwao tuzalishe malighafi kwa ajili ya viwanda vyao. Baada ya miaka mingi ya kujiimarisha, wakaamua kutupa uhuru wa bendera wakituacha kwenye uchumi tegemezi ambao haukuturusu kujitegemea kabisa.
 Baada ya hapo kukaja ukoloni mamboleo. Katika ukoloni mamboleo, mtumwa mwinyewe analima, anatunza, halafu mkoloni mamboleo anakuja anakupanga bei ya mazao yako na wewe unasema ndiyo. Mkoloni akipata fedha  kutokana na mazao aliyonyang'anya, kiasi kidogo cha fedha anakupa na anaita ni msaada. Hicho kiasi chako kidogo cha dhuluma kinachokuja kwako mkoloni mamboleo anakiita msaada. Mkoloni mamboleo anatoa kiasi hicho ili kudumisha uhusiano mzuri kati ya mnyonyaji na mnyonywaji.
 Katika nchi ambamo hata kiongozi wa nchi anachekelea kupewa hicho kiasi kinachoitwa msaada, hakutakuwa na maendeleo hata siku moja.
 Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania, tusijivunie kuona mheshimiwa Kikwete anaongea na balozi wa Marekani akiahidiwa kitu kinachoitwa misaada, hapo wanaweka mikakati ya kuendeleza hali yetu ya kunyonywa! Jana kuona vile ilitakiwa tusikitike siyo kufurahi na rais alitakiwa asijigambe kwamba tunaahidiwa kitu kinachoitwa misaada.
 Hapo alitakiwa baada ya kuongea tu, aseme, jamani mnaona unyonge tulionao? halafu kinachofuata alitakiwa awaambie wananchi namna alivyojipanga kuondoa hali duni na nyonge tuliyonayo kwa kutumia vizuri raslimali zetu hapa nchini.
 Watanzania tubadilike!!! TUWEKE MIKAKATI YA KUJITOA KWENYE MAKUCHA HAYA YA WAZUNGU. TUKATAE UFISADI maana huo ndo unaowakaribisha wazungu waje kuchukua madini yetu kwa bei ya kutupa maana kwetu ni shamba la bibi. Waangalizi wa shamba hilo ndo hao mafisadi. Mafisadi hao wanachukua chao mapema na makapi wanampelekea bibi. Bibi hajui kunachoendelea shambani kwa kuwa miguu yake ni midhaifu hawezi kufika shambani kwa kutembea.
 Unapofika wakati hawa mafisadi tuwaondoe jamani, hawafai. Tuwapeleke wengine ambao hawana tabia ya kifisadi!www.facebook/Expedito Mduda

1 comment:

JAIROS EMC said...

hongera kaka kwa kuwa na mtazamo huo.
Asante kwa kuwafundisha watanzania mema yahusuyo nchi yao.
Karibu sana duniani kunako kero zisizojibiwa na jukwaa la siasa wala magazeti.
Changamoto hiyo kwako kaka
Mdogo wako Mwakavindi Jairos EMC Mwakavindi