Thursday, October 21, 2010

TUACHE MAWAZO MGANDO

    Ndugu Watanzania wenzangu mnaoipenda nchi yetu, naomba wote kwa pamoja tufunge mikanda kuelimisha watu fulani ambao inaonekana mawazo yao ni ya zamani sana na inaonekana elimu waliyoipata waliipata kwa njia moja inayoitwa "indoctrination". Katika njia hii ya kupata uelewa fulani, mtu hupewa na kuaminishwa kitu fulani ambacho hicho atakisimamia mpaka hata afe lakini haachani nacho hata kidogo. Mtu huyo akiulizwa aeleze sababu za kung'ang'ana na hicho kitu mara nyingi haelezi vilivyo ila huishia kutetea na pengine ugomvi na yeyote anayekuwa tofauti naye katika mawazo.
    Jamani hivi inahitaji madarasa mangapi kuelewa kuwa duniani hapa wati hawafanani kwa sura na hata kwa mawazo? Inahitaji nini kujua kuwa kila binadamu hapa duniani ana kasoro zake ingawaje kuna tofauti katika uwingi wa kasoro kati ya mtu na mtu?
    Haya jamani. Jana magazeti yameandika kuwa Serikali inayatishia magazeti ya mwana Halisi na Mwananchi kuwa yatafungiwa sababu eti yanaichonganisha serikali na wananchi wake. AJABU! Hivi kusema kinyume na ulichopenda waseme ni uchonganishi? Kwa kweli ni ajabu kidogo. Ukiwa mtaani na ukakuta watu wamekaa wanaongea, utaona kuwa kila mtu anakuwa na wazo lake huyu hivi na yule vile. Sawa kwa kuwa hatufani!
     Magazeti hayo yaliyotajwa hayachonganishi ila nahisi mara nyingi yanaandika kile ambacho wakubwa wengi hawapendi kiandikwe. Hawapendi kiandikwe kwa kuwa hawajafanya kazi waliyotumwa na wananchi wakafanye. Wafikiria: Mbona magazeti haya yanaanika uovu wetu, tufanye nini kuyazima. Kama kweli magazeti haya yanaichonganisha serikali na wananchi ni habari ipi wameisema imechonganisha!!
Nawashauri serikali ifanye kile walichotumwa na wananchi waone magazeti yataandika nini. Hivi kama serikali imejenga daraja na inatoa elimu bure kwa wananchi na inashughulikia mafisadi ipasavyo kwa nguvu zote, itawezekana magazeti hayo kuandika kinyume na hapo kweli wakati matunda yanaonekana na wananchi wenye!HAPANA.
      Ili tuweze kumudu haya yote tunahitaji serikali safi. Usipokuwa msafi kila unakopita, kila unachosikia unalalama na kulalamika tu eti wananisema! TUAMKE.
      Pia kuna Watanzania mmoja mmoja wananichekesha sana. Hivi eti nyie watu hamuelewei kuwa mwalimu Nyerere naye alikuwa binadamu na kile alichoamini na kupigania si wote walikipokea? Kuna mtuwa ajabu na ajabu kweli na amenishangaza na kweli. Nasema amenishangaza kwa kuwa inaonekana ameenda shule lakini bado anaamini kuwa mtu yeyote aliyetofautiana na mwalimu Nyerere alau katika mfumo wa ujenzi wa taifa letu ni mdhambi kabisa na si tu wa kumfuata. Huyu jamaa amesoma lakini kichwani ana mawazo ya mgando kabisa.
   Mwalimu Nyerere, baba wa taifa letu, alifanya kazi kubwa sana kuikomboa tanganyika yetu toka kwa mkoloni na akatafuta mwelekeo wa taifa letu katika kukunza uchumi. Alijaribu na akafanikiwa kiasi fulani lakini pia yeye kama binadamu alishindwa hapa na pale na hili yeye mwenyewe anakiri hivyo.
   Kwa kuwa hakuwa malaika, kuna watu pia walioona mwelekeo aliochukua ulikuwa hauwaridhishi na hivyo hawakuwa pamoja naye kwa kila kitu kwa maana ya kuwa walikubaliana katika hili na wakatofautiana katika lile. Nani alikuwa sahihi, hilo hatujui!!
Tofauti hiyo haikumanisha kuwa watu waliotofautiana na mwalimu hawakuwa wazalendo, HAPANA. Walikuwa wazalendo tena wazuri kabisa na ndio maana wakajipambanua wakaonekana wametofautiana naye. Hivyo kwa mtu yeyote anayefikiri kutofautiana na mwalmu ilikuwa dhambi ana mawazo yaliyoganda kabisa.
     Huyu ndugu yetu Sheka ninamuomba atueleze zaidi kwa uwazi anachoona Mtei alikosa sana kwa kutokuwa pamoja na mwalimu katika mambo fulani kama kweli tofauti hiyo ilikuwepo. Je, babu yake Sheka hayupo katika historia ya ukombozi, hivyo tuseme hakuwa mzalendo? Hata kama Mtei hakushiriki kikamilifu katika mapambano ya kuikomboa Tanzania, kama ni kweli hivyo ndivyo, ni mawazo ya mbali sana kuona hilo linamwondolea haki ya kuanzisha chama. Kwani wote walowahi kushika madaraka walikuwepo wakati wa ukombozi miaka hiyo? SHEKA aachane na mawazo hayo. Labda kwa hayo aliyosema atuambie kwa uhakika masterpan ya CHADEMA ambayo sisi hatuifahamu ili tufahamu tupime. Lakini kama ni hiyo stori aliyokopi na kupesti, haijafanya chochote.http://www.mrmduda.blogspot.com
 

No comments: