Sunday, December 19, 2010

CCM WATANGULIZE MASLAHI YA WANANCHI

  Kuna mambo mengi sana yanayowachefua Watanzania sasa. Harakati zilizoendeshwa ili kutusaidia kupata uhuru zililenga kumkomboa Mtanganyika kuondokana na umaskini, ujinga na maradhi.
   Leo hii baada ya miaka 49, Watanzania wamekuwa na hali mbaya nafikiri kuliko hata hali waliyokuwa nayo miaka ya sabini. Sisi Watanzania tukae tufikiri kwa makini ili tujue kosa letu liko wapi.
   Kama kweli tunataka kuondokana na shida tulizonazo tusiogope kuambiana ukweli pale mmoja wetu anapotusaliti na kusababisha turudi nyuma kimaendeleo.
   Kwanza kabisa tunasikia miaka hiyo kulikuwa na chama kilichoitwa TANU na baadaye jina likawa CCM. Chama hiki kimekuwa madarakani toka tunapata uhuru. Kama chama hiki kimekuwepo madarakani muda huo wote, na serikali yake ndio ilikuwa na wajibu wa kuondoa matatizo Tanzania na hayo matatizo hayajaondoka lawama ziende kwa nani. Kwa uelewa wangu CCM wabebe lawama ya kutufanya Watanzania tubaki na hali mbaya mpaka leo.
   SERIKALI ya CCM inakiri kwamba Tanzania bado tu maskini sana. Hii ilionekana pale mwenyekiti wao aliposema hawezi kuongeza kima cha chini cha mshahara kufikia Tsh.350000.
   Hivi jamani Watanzania, nani hajui maisha ya leo hapa Tanzania mtu hawezi kuishi kwa dola mbili. Sasa fikiri serikali inalazimisha watu wake waishi kwa dola mbili wakati haiwezekani. Je, hapo utategemea umkute mtu au mfanyakazi ana afya inayomwezesha kufanya kazi kwa furaha? Jibu la kweli ni hapana. Mtu akiwa ofisini ataendelea kufikiri namna ya kupata chochote kwa njia nyingine ili aweze kutimiza mahitaji kule nyumbani.
   SERIKALI imeshindwa kusimamia raslimali za taifa letu ili wananchi wake wafaidike nazo. Hakuna mtu anayebisha hilo. Hebu tuone fedha zinazotumika kuzalisha umeme. IPTL, RICHMOND na mengine mengi yametuchukulia fedha nyingi ajabu. Toka miaka hiyo yote ya uhuru tumeshindwa nini kuhakikisha sisi wenyewe tunaazisha miradi mikubwa ya kuzalisha umeme unaotutosha badala ya kukodi makampuni hewa kama RICHMOND. Hiki ni kielelezo kwamba serikali ya CCM imeshindwa kufanya kazi.
   Mifano mingine midogo kabisa ni kama pale serikali iliposhindwa kutuambia wananchi kampuni za kagoda ni za nani maana nazo zilichukua mabilioni ya walipa kodi. Bado hatujakaa sawa tunaambiwa tunatakiwa kuilipa DOWANS Tsh. bilioni 185. Hivi jamani hawa watawala wetu wametupeleka wapi mpaka tunaingia hasara hizi. Tumefanya uchaguzi jana tu. Wananchi wamechagua viongozi wao. Kwa kuwa kumekuwa na usiri na kutoaminiana kwa mazingira ya uchaguzi kugubikwa na mazingira ya wizi leo hii kesi za kupinga matokeo sehemu mbalimbali zimefunguliwa. Kwa hilo tu tayari tunatakiwa kutoa Tsh. zaidi ya bilioni mbili.
  Mnafikiri kwa hayo yote yanayoendelea kuna siku maendeleo yatakuja Tanzania. Kweli kwa mtindo huo ni ngumu sana.
   Juzi tumemsikia waziri mkuu anakataa gari ambalo limekwisha nunuliwa. Hivi huko serikalini hakuna mtu mwenye kauli moja ambaye akitoa basi waliopo chini yake wanatekeleza? Nauliza hivi kwa sababu ni muda mrefu sasa waziri mkuu alitamka kuwa magari ya bei kubwa na ya starehe yasinunuliwe na fedha hizo zielekezwe kununua matrekta madogo. Ilikuwaje wanunue aina ya gari la bei kubwa ambalo tayari waziri mkuu alishaagiza kutonunuliwa.
   Magari ya serikali yanatumika mitaani utafikiri ya watu binafsi. Hakuna anayekemea tabia hiyo. Mafuta yanayotumika siyo kodi ya wananchi. Kwa kweli ndugu zangu uzalendo wa nchi yetu umepungua sana. Hakuna anayemfikiria mtu wa chini sasa. Mmoja akishapata anawasahau kabisa wananchi wa chini.
   Ili Tanzania tuendelee tuwakute waliotuacha wakati tulianza pamoja, tunatakiwa kukaa chini kwanza tumtambue msaliti na huyo awe adui wetu sote tumuondoe na tujipange upya kwa mwendo mkali zaidi. Kama tutazidi kuwa naye huyu hata tujitahidi ataturudisha nyuma tu maana ni msaliti.
   Tutafika hapo tukiwaacha wananchi wawachague viongozi wao wanaowataka. Hakuna haja ya kulazimisha wananchi kupewa viongozi wasiowataka.