image slider

HUDUMA TUNAZOZITOA
Watengenezaji wa mashine za kuangulia vifaranga vya kuku
Wauzaji wa vifaranga vya kuku
Ushauri wa ufugaji wa kuku
Mashine za kuangulia vifaranga vya kuku
Wauzaji wa vifaranga vya kuku
Mashine za kuangulia vifaranga vya kuku

Wednesday, January 13, 2016

UFUGAJI WA KUKU

UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI

Idadi ya wanyama wanaofugwa kwa chakula imezidi ile ya binadamu zaidi ya mara mbili kote ulimwenguni. Kuna maelfu ya wanyama kote duniani ilihali ni wachache tu wanaoweza kufugwa. Kati ya hawa wanyama, ni aina nne (Ng'ombe, kondoo, mbuzi na kuku) wanaochukua asilimia 95% ya wanyama wote wanaofugwa. Wanyama hawa hupatikana katika nchi za hari kwenye nyanda za chini. Lakini kati ya mifugo hawa, kuku ni maarufu katika nchi za hari na hata kote ulimwenguni.
Lengo la makala haya ni kutoa maelezo ili kusaidia wafugaji wa kiwango kidogo katika nchi
zinazostawi, katika kupunguza umaskini. Sehemu ya kwanza (I) itatoa maelezo kuhusu ufugaji na
hasa ufugaji wa kuku, Sehemu ya pili (II) itaangazia maswala yafuatayo katika kuinua hali ya uchumi
kwa kufuga kuku:
1. Kuendeleza ufugaji wa kuku za kienyeji kwa kutumia njia zisizohitaji gharama nyingi.
2. Kutafuta mbinu na njia muafaka za kuzalisha viwango vya kuku bora kwa njia ya kiasili.
3. Matumizi ya njia za kiasili au zile zisizo gharimu pesa nyingi kutibu na kuzuia magonjwa ya
kuku.

SEHEMU YA I: MAELEZO KUHUSU UFUGAJI WA KUKU KATIKA NCHI. ZINAZOENDELEA

NAFASI YA MIFUGO

Licha ya kukosa mashamba makubwa ya kuendeleza ufugaji wa ng'ombe, jamii nyingi katika nchi za
hari (tropics) hupata nafasi ya kufuga kuku kwa kiwango kidogo. Idadi ya wanyama wanaofugwa
huongezeka sambamba na ile ya watu. Idadi ya watu inapoongezeka ndipo ile ya mifugo huzidi.
Idadi kubwa ya watu huhitaji chakula kingi na matumizi huongezeka, hivyo basi watu hufanya bidii
kuzalisha chakula na mapato kutoka kwa shamba.
Ufugaji wa ng'ombe na wanyama wanaohitaji lishe kwa wingi huhitaji kiasi kikubwa cha shamba ili
kupanda mimea na lishe la mifugo. Ukilinganisha na ufugaji wa kuku, utahitaji mabaki ya vyakula
na sehemu ndogo ya shamba. Ufugaji wa kuku umeweza kunawiri hata pasipo fedha.
Katika nchi za hari ufugaji wa kienyeji hautahitaji kazi nyingi, kazi hii hufanywa na akina mama na
watoto. Kwa kawaida katika nchi hizi kazi nyingi za nyumbani hutekelezwa na mama. Vyakula vya
kuku vyaweza kutoka kwa: 1) Mabaki ya chakula, 2) Mabaki ya mimea, 3) Mabaki kutoka jikoni
na 4) Vyakula vya kujitafutia (kwa mfano kwekwe, mbegu, wadudu, nyongonyongo, n.k). Mfumo
wa kufuga kuku kwa njia ya kienyeji hutumia viungo vinavyopatikana kwa urahisi na kuimarisha hali
ya kiuchumi na chakula bora kwa jamii.
Ni muhimu sana kufuga mifugo hata ikiwa ni kwa kiwango kidogo kwa sababu ya 1) Chakula bora
na kuongeza mapato ya jamii kwa viwango vya kuridhisha; 2) Mifugo ni hakiba au banki, faida yake
huzaana tu kama riba ya benki; 3) Mifugo yaweza kuuzwa ili kugharamia karo ya wanafunzi,
malipo ya hospitali, gharama nyingine za nyumbani na hata shambani; 4) Kwa matumizi ya kijamii
(kwa mfano kulipia mahari, shughuli za kidini, n.k); 5) Mifugo husaidia katika kukabili wadudu,
kwekwe na kuimarisha rutuba kutokana na mbolea ya kinyesi. Ni bayana kwamba mifugo ni
muhimu sana kwa mkulima yeyote yule

UMUHIMU WA UFUGAJI WA NJIA YA KIENYEJI

Ufugaji wa kuku katika nchi zinazostawi waweza kugawanywa mara mbili: 1) Ufugaji wa
kitamaduni au kienyeji pasipo kuwepo gharama, na 2) Ufugaji wa kisasa unaohitaji fedha nyingi.
Ufugaji wa viwango vikubwa kwa kuzingatia mfumo wa kisasa ni maarufu katika kuzalisha kuku wa
nyama na wale wa mayai. Mfumo huu hujumuisha asilimia ndogo sana ya aina ya ufugaji.
Itafahamika kwamba mfumo wa kisasa haujaadhiri ule wa kienyeji. Idadi kubwa ya watu katika nchi
za hari hutegemea mfumo wa kienyeji kwa nyama na mayai.
Mfumo wa kisasa huhitaji pesa nyingi za kununua vyakula vya kuku. Aidha mfumo wa kisasa huhitaji kazi nyingi ili kutekeleza. Mfumo wa kisasa
umefaulu katika nchi zilizostawi kutokana na hali nzuri ya kiuchumi katika kuzalisha (kuku wa hali
ya juu, kuangua vifaranga kwa stima, vyakula vilivyo na madini mengi, vifaa na zana za mashine,
utaalamu wa hali ya juu n.k). Haitafaa sana kuanzisha mfumo kama huu katika vijiji vya mataifa
yanayostawi.
"Mageuzi" katika ufugaji (kuambatanisha mfumo wa kisasa pamoja na ule wa kienyeji) yamefanyiwa
majaribio katika mataifa yanayostawi tangu miaka ya 1950. Matokeo ya kuku wapatao 200 hadi 300
kwa shamba moja hayajawai kufaulu. Hasara imepatikana na waweza kuona nyumba zilizokuwa na
kuku bila chochote, pesa nyingi zimepotea na kuku hawapo.
Mfumo wa kienyeji ni bora (Katika hali ya kiuchumi) iwapo idadi ya kuku haitazidi kuku 50. Ni
rahisi kuweza kuwatunza kuku, kwani hakuna gharama nyingi. Iwapo vyakula au zana za kisasa
zitanunuliwa, basi haitakuwa kwa viwango vikubwa. Mazao ya nyama na mayai yataleta faida.
Sehemu nyingi katika mataifa yanayostawi hakuna stima, katika nchi za hari, ufugaji kwa kiwango
kidogo umeweza kufaulu na kuimarisha uchumi.

FAIDA ZA UFUGAJI WA KUKU KWA NJIA YA KIENYEJI

Faida za uzalishaji kuku ili kuimarisha uchumi kwa njia hii zimepuuzwa na viongozi na wafadhili.
Kuku huleta faida kwa jamii kama tulivyoona katika sehemu ya I. Zaidi ya hayo, ufugaji wa kuku waweza kuimarishwa pasipo gharama nyingi ukilinganisha na mifugo wengine.
· Hutupatia fedha kwa kuuza nyama na mayai
· Mayai ni chakula kilicho na madini muhimu na kisicho ghali katika soko lolote. (madini kama methionine na cystine), madini haya ni muhimu sana kwa afya ya watu hasa watoto wachanga. Pia hutupatia protini.
· Kinyesi cha kuku ni mbolea safi
· Kiwanda asilia cha kutotoa vifaranga
· Gharama za kuanzisha na kuendeleza ni nyepesi
· Kitoweo chepesi na rahisi kwa wageni, kitoweo hakihitaji hifadhi hutumika mlo mmoja au miwili na kumalizika
· Jogoo hutumika kama saa inapowika
· Manyoya ya kuku hutumika kutengenezwa mapambo mbalimbali, mito na magodoro
· Kuku wanahisimu wadudu waharibifu
Kuku ndiye mnyama wa kipekee anayeweza kuishi mahali popote hapa ulimwenguni bila kuadhiriwa
na viwango vya hali ya hewa. Ufugaji wa kuku ndio shughuli inayofanyika kwa wingi duniani kuliko ufugaji wa aina yeyote. Kuku hunawiri vyema katika nchi za hari kutokana na uwiano uliopatikana wakati wa mwanzo binadamu alipofuga Asian jungle fowl aina ya kuku-mwitu. Mayai pia yaweza kuhifadhiwa kwa urahisi na huchukua nafasi ndogo kuliko aina ya bidhaa zozote za mifugo. Mayai yaweza kuwekwa mahali kwa muda mrefu bila kuhitaji barafu. Hautahitaji kuhifadhi kuku kwa njia yoyote, kwani nyama yake hupatikana pale unapohitaji kwa kuchinja.

Upungufu wa kuku wa kigeni ukilinganisha na wale wa kienyeji ni kama ufuatao:

• Kuku wa kigeni hawawezi kukalia na kuangua mayai, hivyo basi wahitajika kununua vifaranga (gharama);
• Vifaranga wa kigeni huhitaji utunzaji maalum na vyakula maalum (gharama);
• Kuku waliozalishwa kwa njia ya kisasa huhitaji chakula kingi ili kutaga mayai (gharama);
• Kuku wa kisasa huhitaji zaidi kuchanjwa dhidi ya magonjwa (gharama)ukilinganisha na wa kienyeji (japo nao huhitaji chanjo);
• Kuku wa kutaga mayai huhitaji mwangaza wa stima (saa 14 kwa siku) ili kutaga mayai (gharama)
Kwa kuongezea, rangi ya nyama na mayai ya kuku wa kienyeji huvutia kuliko ile ya kuku wa kisasa.
Hivyo basi jaribu kuendeleza na kuhimiza ufugaji wa kuku za kienyeji.
Iwapo mkulima ana jogoo mmoja na kuku kumi na mbili, basi kila mwezi waweza kupata kuku
akikalia mayai 10-12 kwa mwezi (mayai yote kwa wakati mwingi hayataanguliwa) kuna hakikisho la
kupata vifaranga vinne kila mwezi. Kuku mzima atachukua miezi minne kuchunga vifaranga
walioanguliwa. Kwa hivyo, kati ya kuku wote kumi na mbili kila mara kutakuwa na kuku wanne
wakitunza vifaranga, huku wale wengine wanane wakitaga mayai.
Kuku waliofugwa kwa njia ya kitamaduni hupata vyakula vyao kwa kutafuta mbegu, wadudu
nyongonyongo, n.k; Lakini kuku hawa hukosa vyakula vya kutosha vilivyo na nguvu ili waweze
kutaga mayai. Vyakula vya kutoa nguvu daima huwa ni haba.
Waweza kuwalisha kuku kwa nafaka ili wapate chakula cha nguvu (mfano kilo moja ya nafaka
iliyopondwa kila siku kwa kuku 10), nafaka hii yapaswa kuwa kavu. Vifaranga wapewe kiasi kidogo
cha nafaka au mchele wiki za kwanza. Kuku wanaolishwa nafaka baada ya kujitafutia chakula nje
huongeza idadi ya mayai (kutoka asilimia 20-25% hadi 40-50%). Kuna umuhimu wa kuhifadhi
nafaka kama lishe badala ya kuuza kwani utapata mayai mengi ambayo baadaye utaweza kuuza.
Hautahitaji kununua vyakula vya protini kwani kuku hujitafutia lishe la protini.
Ikiwa hauna nafaka, waweza kutumia vyakula vya mzizi au ndizi. Vyakula vya aina hii hata hivyo,
huwatatiza kuku wanapovitonogoa, kiwango cha mayai sio kikubwa kama cha wale wanaolishwa
nafaka.
Kwa kuwalisha kuku kwa nafaka utapata hakikisho la mayai manne kwa siku kutoka kwa wale kuku
wanane. Iwapo hakuna nafaka, kati ya kuku wanane wanaotaga utapata mayai mawili tu kwa siku.
Ni bora kutumia nafaka hii kama lishe kuliko kuuza na hatimaye kununua vyakula vya dukani.
Kuku kumi na mbili na jogoo mmoja wanaolishwa kwa kilo moja ya nafaka kila siku waweza
kuelezwa hivi:
• Waweza kuuza kuku wanne kila mwezi na kujaza pengo hilo na wale vifaranga (vifaranga
wanne huanguliwa kila mwezi) na
• Dazani kumi za mayai kila mwezi (mayai manne kila siku).
Kwa mwaka mmoja waweza kukadiri ile faida utakayopata na vile hali ya kiuchumi yaweza
kuinuliwa katika mataifa yanayostawi.
Hata hivyo faida hii haitaafikiwa iwapo magonjwa
hayatazuiwa au kukabiliwa kama ifuatavyo.

TEKELEZA UTARATIBU WA KUZUIA MAGONJWA

Magonjwa ndio husababisha hasara katika mfumo wa ufugaji wa kuku. Kuku waliochanjwa dhidi ya
magonjwa hudumisha afya bora. Jaribu kila mara kuzuia magonjwa, kwani kuzuia ni bora kuliko
kuponya. Kinga yaweza kutolewa mara kwa mara (kila baada ya miezi mitatu) dhidi ya magonjwa
yafuatayo:

Ugonjwa wa Newcastle

Ugonjwa huu ndio huadhiri kuku na kusababisha hasara katika nchi za hari. Virusi vya ugonjwa huu
huenea kwa kasi na rahisi kiasi cha kusababisha vifo kwa asilimia 100%. Dalili za kwanza ni shida
ya kupumua na kung'amua hewa, sauti kama ya kikohozi na kutokwa mate. Kinyesi chaweza kuwa
na rangi ya kijani kibichi. Hadi sasa hakuna dawa.
Waweza kuzuia ugonjwa huu kwa kutoa chanjo. Dawa za chanjo hupatikana kote ulimwenguni hata
katika nchi za hari kwenye vipimo vya vitone mia moja. Madawa haya yaweza kuhifadhiwa kwa
muda. Waweza kuweka kwa wiki moja mbali na jua au joto kali (Chanjo hii ni ya kipekee, kwani
aina nyingine ya chanjo huwekwa kwa friji). Waweza kutoa chanjo kwa kutia vitone kwenye
mdomo. Kuku wote (wakubwa kwa wadogo) wapaswa kupewa chanjo baada ya kila miezi mitatu.

Minyoo

Minyoo kama chango (roundworms) na tegu (tapeworms) huadhiri kuku wa kienyeji. Kuku hukosa hamu ya chakula, mayai hupungua na magonjwa mengine hushambulia. Ni bora basi kutoa minyoo.
Mchanganyiko wa madawa ya aina tatu ndio hutumiwa kuangamiza minyoo, madawa haya ni
piperazine, phenothiazine na butynorate. Madawa haya hupatikana kama vidonge (tumia kidonge 1
kwa kuku mzima na 1/2 kwa vifaranga). Iwapo hautapata dawa hii, waweza kutumia Panacur au
dawa nyingine ya kuangamiza minyoo. Wapatie kuku dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu.

Wadudu

Wadudu kama chawa au utitiri husumbua kuku katika ufugaji wa kienyeji. Chawa au utitiri
husababisha harara ya ngozi, kuku walio adhiriwa hupata shida na kukosa usingizi. Hali hii
hupunguza kiwango cha mayai na uzito wa kuku.
Tumia asilimia 5% ya unga wa malathion kwa kupulizia kuku (puliza kwa chupa uliyo toboa
mashimo) pulizia kila kuku ili kuzuia chawa na utitiri (kilo moja ya unga huu yaweza kutibu kuku
150). Pulizia dawa hii baada ya kila miezi mitatu, waweza kupuliza kwa wakati mmoja wa kutoa
chanjo na dawa zilizotajwa hapo juu. Puliza unga huu pia kwenye viota vya kuangulia mayai.
Waweza kutayarisha 5% ya malathion kwa kuchanganya 25% ya unga wa malathion (kiwango cha
kilimo) na sehemu nne za jivu kutoka jikoni.

Magonjwa ya mapafu

Magonjwa ya mapafu huadhiri njia inayopitisha hewa na kuambatanisha mate na sauti kama ya
kikohozi. Ugonjwa huu huenea polepole. Uambukizanaji pia hutokea kwa polepole na vifo sio kwa
wingi. Hata hivyo, kutaga mayai na uzito hupungua. Shida hii yaweza kusambaa hata kutoka mahali vifaranga huanguliwa hadi pale walipouzwa.
Tylosin19 ndio dawa inayoweza kutibu magonjwa ya mapafu. Kiasi cha 35mg ya tylosin hutosha
kuku mmoja (kiwango hiki hufaa kuku na hata vifaranga) dawa hii husimamisha madhara kutokana
na magonjwa ya mapafu. Tibu kuku kila baada ya miezi mitatu, waweza kutekeleza kwa wakati
mmoja wa kutoa kinga na kuangamiza minyoo. Tylosin hupatikana kwa pakiti ndogo ya 4gm.
Waweza kutayarisha dawa hii kwa kutumia maji na 35gm ya tylosin (gramu nne kwa vikombe viwili
vya maji), kiasi hiki chaweza kutolewa kwa vitone kwa kila kuku

KWA UFUPI (SUMMARY)

Kabila za Kuku

Si rahisi kupata kabila halisi (pure breed) au kizazi halisi (pure line) za kuku wa kienyeji kutokana na mwingiliano wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao. Lakini hata hivyo baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kutokana na maumbile yao kwa mfano

1. Kuchi

Warefuna wenye kusimama mgongo ukiwa wima
Wana manyoya machache mwilini na vilemba vyao ni vidogo
Majogoo huwa na wastani wa kilo 2.5 na mitetea kilo 1.8
Mayai gram 45

2. Ching'wekwe (Umbo dogo)

Hupatikana zaidi Morogoro na umasaini
Majogoo kilo 1.6
Mitetea kilo 1.2
Yai gram 37
kuku hawa wanafaa sana kwa biashara ya mayai kwa kuwa hutaga mayai mengi sana.

3. Umbo la Kati

Majogoo kilo 1.9
Mitetea kilo 1.1
Mayai gramu 43
Hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa Mdondo (New Castle)

4. Singamagazi

Hupatikana zaidi Tabora
Majogoo wana rangi ya moto na mitetea rangi ya nyuki
Majogoo kilo 2.9
Mitetea kilo 2
Mayai gramu 56

5. Mbeya

Wanapatikana Ileje Mbeya na asili yao ni Malawi
Mjogoo kilo 3
Mitetea kilo 2
Mayai gramu 49
Uwezo wao wa kuatamia mayai na kuangua ni mdogo sana ukilinganisha na kuku wengine

6. Pemba

Maumbo ya wastani na miili myembamba
majogoo kilo 1.5
mitetea kilo 1
mayai gramu 42

7. Unguja

Hawatofautiani sana na wa Pemba
Vilemba vyake ni mchanganyiko- vidogo an vikubwa
Majogoo kilo 1.6
Mitetea kilo 1.2
Mayai gramu 42