image slider

HUDUMA TUNAZOZITOA
Watengenezaji wa mashine za kuangulia vifaranga vya kuku
Wauzaji wa vifaranga vya kuku
Ushauri wa ufugaji wa kuku
Mashine za kuangulia vifaranga vya kuku
Wauzaji wa vifaranga vya kuku
Mashine za kuangulia vifaranga vya kuku

Tuesday, October 26, 2010

KILA MMOJA WETU AHAKIKISHE ANASHIRIKI KIKAMILIFU KUIKOMBOA NCHI YETU

Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wa bendera kutoka kwa Waingereza. Ingawa tulio wengi hatukuwepo muda huo, tunajua kuwa wazee wetu walidai uhuru kwa madhumuni ya kuhakikisha tunajitawala ili tujifanyie mambo yetu tunayoyataka bila kushinikizwa na nyingine na pia kuona wananchi wanapata mamlaka ya kuendesha nchi yao.
Kwa hali hiyo kila Mtanganyika alikuwa na matumaini makubwa sana. Kwa hali ya kawaida binadamu ana mahitaji muhumu matatu. Nayo ni chakula, malazi na mavazi. Hivyo mtu yoyote utakayemwona anashughulika ujue yuko katika mchakato wa kuhakikisha anapata hayo mambo matatu bila shida.
Mungu alipomwumba mtu alitaka kila mmoja afaidike na raslimali za pale alipozaliwa. Kwa maana hiyo Mungu alikusudia Watanzania wafaidike na mali zao zilizopo Tanzania.
Ubinafsi ulipoanza, ndipo historia ya dhuluma ilipoanza. Tunasikia mambo ya biashara yalianza kila mtu akitafuta faida kwa kufanya dhuluma kwa mwenzake na hivyo hiyo ikaonekana kwamba ndani kwa kila mtu kuna kitu fulani kinachomssukuma kukusanya mali nyingi kwa kufanya wizi fulani. Hii haikuwa kusudi la Mungu!
Tabia hiyo ni mbaya sana tena nafikiri kwamba ubinafsi ni dhambi. Pale unapofanya dhuluma na hasa kama mtu umekabidhiwa mali ya jumuia wewe unakuwa ni muuaji sawa tu na yule anayechukua panga na kumkata mtu mwingine kwa ajili ya kunyang'anya mali.
Ndugu Watanzania, nchi yetu imetumbukia katika dimbwi kubwa la ubinafsi na wizi mkubwa sana. Viongozi wetu tuliowaamini na kuwapa dhamana wamejisahau na wamefikiri mali yote ni yao na hivyo hakuna haja ya kuwatumikia wananchi ila ni kuhakikisha wanafanya jitihada yoyote kuhakikisha wanashinda na wanabaki madarakani waendelee kuiba na kujinufaisha wenyewe.
Kama vile imesemwa mwanzo kwamba lengo la kudai uhuru kutoka kwa wale waliotangulia kuwa wabinafsi na kuja kututawala na kuiba mali zetu ilikuwa ni kuona mali zetu zinatufaidisha wote. Kitu cha ajabu ni kuwa baada ya kupata uhuru watu wamesahau malengo hayo na wanachofanya ni kuviziana na kila mmoja kunyakua kile kilichopo mbele yake na kuondoka.
Mambo haya yanadhihirika tunapoona viongozi wetu wanalimbikiza mali kupindukia wakati huo Watanzania wengi wakiwa hata hawawezi kupata yale mahitaji muhimu hata kwa kiwango cha chini kabisa.
Serikali yetu ya muhula wa nne imefanya mambo ya ajabu ya ubinafsi pengine kuliko serikali zote zilizotangulia. Hapa ninasema hivyo kwa sababu tumeona viongozi wetu wakiwa mahakamani kwa kesi za kukwapua mali za wananchi. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na matarajio ya wengi.
Eti jamani, katika hali ya kawaida imewezekanaje mtu kupatikana na wizi huo lakini bado akaendelea kuwa katika ofisi ya umma na baadaye kupigiwa chapua la kuchaguliwa tena ili arudi katika nafasi ile ile aliyotumia kuiba mwanzoni?
Hivi sisi Watanzania hatuwezi kuona, kuhisi, kusikia wala kunusa!
Pengine tuseme hivi hatuwezi kuona haya yanayotendeka wazi wazi. Mtu anakuibia halafu baadaye anaomba umchague tena arudi madarakani kwa kukuletea komedi ili usahau lile alofanya mwanzo. Je, sisi Watanzania ni watu wa aina hiyo?
Ndugu zanguni, bila kuwa wanafiki mnajisikiaje pale familia moja inapotumia jasho la mlipa kodi ili kufanya mambo ya kifamilia yasiyo ya msingi kwa ustawi wa taifa letu. Mume ndege, mke ndege, watoto magari ya bei kali. Hizi ni mali za nani hasa.
Watanzania, kwa pamoja tuinuke tukapige kura ili tuwatose hao wasiotufaa.
Tuanze na kuona mali zetu zinavyoliwa na watu wachache wasio na uchungu na nchi yetu.
Mambo ya msingi yanayotakiwa yafanyike ili sisi tujikomboe na umaskini tulio nao ni kuwekenza katika elimu. Hii ina maana elimu ni ufunguo wa maisha. Mtu aliyeenda shule akasoma na kuelewa anaweza kupata chakula bora, malazi na mavazi safi. Kwa maana hiyo kama elimu ndio msingi wa maisha kila mtoto wa Mtanzania anatakiwa apewe elimu bora. Ili kuweza kutimiza hili utoaji elimu hautakiwi kuwa na vikwazo vingi tunavyoona sasa. wengi ni mashahidi wa ukweli kwamba watoto wa walala hoi wameishia darasa la saba si kwa sababu hawana uwezo wa kuendelea juu hapana ila ni kwa sababu ya kutokupata fursa ya kusoma kwa kuwa wazazi wao hakuweza kuwalipia ada na michango mingine. Hii ina maana uwezo wa kifedha ndo kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya elimu nchini kwetu. Je, nani atbisha hilo? Kama tunakubaliana hapo, basi kwetu kiongozi anayetangaza elimu bure ndiye huyo anayetufaa sisi na si mwingine.
Kama nyumba ni sehemu ya mahitaji muhimu ya binadamu, ni kiongozi gani atakayetuwezesha sisi tujenge nyumba tuishi ili tuwe tumepata hitaji hilo la binadamu? Mimi nafikiri ni yule anayekumbuka hata kutuambia tu kwamba ujenzi wa nyumba utawezekana kama vifaa vya ujenzi vitakuwa vya bei ya chini ili wengi wetu tununue na tujenge nyumba. Kuongelea tu ujenzi wa barabara haitoshi maana barabara zinakumbukwa zaidi kwa kuwa hao wanaoiba na kufaidika kibinafsi na mali za nchi yetu ndo wenye magari ya kupitisha hizo barabara. Mimi mlala hoi cha msingi nyumba, elimu, na chakula. Barabara sawa lakini twende kwa vipau mbele ili kinachofanyika kimguse mwananchi wa chini kabisa.
Ili wananchi tuwe na nguvu ya kuleta serikali tunayotaka madarakani tunayo silaha moja kubwa: "KUPIGA KURA". Tusidanganywe ili tupige kura kumpigia mtu eti aliyetoa t-shirt, kofia na mabango. Mabango hayo ni fedha yetu inayotumika vibaya. Tunasema inatumika vibaya maana tungeondoa ubinafsi hiyo fedha iliyotumika kutengeneza mabango ingetununulia vitabu ili tusome tupate elimu bora.
Kwa kweli amini msiamini ndugu zangu, Tanzania yetu kwa sasa inahitaji matengenezo makubwa la sivyo huko tunako enda siko tuliko kusudia kwenda.

No comments: