Sunday, October 31, 2010

SAA YA UKOMBOZI IMEFIKA

Ndugu zangu Watanzania, inaonekana wengi wetu wamegundua kuwa nchi yetu ipo mikononi mwa mafisadi na hivyo tumeamua kuhakikisha kufanya jitihada ya kuikomboa nchi hii kutoka kwenye mikono michafu ya watu hawa wasio na huruma yoyote.
Kila kukicha wamekuwa wakipanda ndege kwenda nje ya nchi kunywa chai na bwana Obama. Wakiwa majukwaani watuambia wamepigiwa simu na Obama. Sisi simu za Obama hatuzihitaji ila tunachokitaka ni maendeleo. Wakiwa majukwaani wanaonyesha mbwembwe kwamba wanaweza sana kucheza na kunengua kumbe sisi hatuhitaji hayo ila maendeleo.
Ndugu zanguni, hatua hii si mbaya! Tumefika mahali na wala tusikate tamaa kabisa ukombozi umekaribia na tunaweza kurudisha nchi yetu mikononi mwetu. Sisi ni wapiganaji tusiochoka!
Katika historia hakuna mpiganaji yeyote aliyeungwa mkono kwa asilimia mia moja! HAPANA! cha msingi hapa ni kutokukata tamaa maana muda wa ukombozi umekaribia.
Hapa zamani walitudanganya kwa maneno matamu eti maisha bora kwa kila Mtanzania kumbe maana yake ni maisha bora kwa kila mwanafamilia ya bwana mkubwa. Ehee, jamani saa ya ukombozi imefika. Tusilale mpaka tuhakikishe nchi yetu ipo mikononi mwetu.
Kumbe mambo si haba! Mafisadi wanatetemeka na matumbo yao moto.
HATULALI MPAKA KIELEWEKE!!!

Tuesday, October 26, 2010

KILA MMOJA WETU AHAKIKISHE ANASHIRIKI KIKAMILIFU KUIKOMBOA NCHI YETU

Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wa bendera kutoka kwa Waingereza. Ingawa tulio wengi hatukuwepo muda huo, tunajua kuwa wazee wetu walidai uhuru kwa madhumuni ya kuhakikisha tunajitawala ili tujifanyie mambo yetu tunayoyataka bila kushinikizwa na nyingine na pia kuona wananchi wanapata mamlaka ya kuendesha nchi yao.
Kwa hali hiyo kila Mtanganyika alikuwa na matumaini makubwa sana. Kwa hali ya kawaida binadamu ana mahitaji muhumu matatu. Nayo ni chakula, malazi na mavazi. Hivyo mtu yoyote utakayemwona anashughulika ujue yuko katika mchakato wa kuhakikisha anapata hayo mambo matatu bila shida.
Mungu alipomwumba mtu alitaka kila mmoja afaidike na raslimali za pale alipozaliwa. Kwa maana hiyo Mungu alikusudia Watanzania wafaidike na mali zao zilizopo Tanzania.
Ubinafsi ulipoanza, ndipo historia ya dhuluma ilipoanza. Tunasikia mambo ya biashara yalianza kila mtu akitafuta faida kwa kufanya dhuluma kwa mwenzake na hivyo hiyo ikaonekana kwamba ndani kwa kila mtu kuna kitu fulani kinachomssukuma kukusanya mali nyingi kwa kufanya wizi fulani. Hii haikuwa kusudi la Mungu!
Tabia hiyo ni mbaya sana tena nafikiri kwamba ubinafsi ni dhambi. Pale unapofanya dhuluma na hasa kama mtu umekabidhiwa mali ya jumuia wewe unakuwa ni muuaji sawa tu na yule anayechukua panga na kumkata mtu mwingine kwa ajili ya kunyang'anya mali.
Ndugu Watanzania, nchi yetu imetumbukia katika dimbwi kubwa la ubinafsi na wizi mkubwa sana. Viongozi wetu tuliowaamini na kuwapa dhamana wamejisahau na wamefikiri mali yote ni yao na hivyo hakuna haja ya kuwatumikia wananchi ila ni kuhakikisha wanafanya jitihada yoyote kuhakikisha wanashinda na wanabaki madarakani waendelee kuiba na kujinufaisha wenyewe.
Kama vile imesemwa mwanzo kwamba lengo la kudai uhuru kutoka kwa wale waliotangulia kuwa wabinafsi na kuja kututawala na kuiba mali zetu ilikuwa ni kuona mali zetu zinatufaidisha wote. Kitu cha ajabu ni kuwa baada ya kupata uhuru watu wamesahau malengo hayo na wanachofanya ni kuviziana na kila mmoja kunyakua kile kilichopo mbele yake na kuondoka.
Mambo haya yanadhihirika tunapoona viongozi wetu wanalimbikiza mali kupindukia wakati huo Watanzania wengi wakiwa hata hawawezi kupata yale mahitaji muhimu hata kwa kiwango cha chini kabisa.
Serikali yetu ya muhula wa nne imefanya mambo ya ajabu ya ubinafsi pengine kuliko serikali zote zilizotangulia. Hapa ninasema hivyo kwa sababu tumeona viongozi wetu wakiwa mahakamani kwa kesi za kukwapua mali za wananchi. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na matarajio ya wengi.
Eti jamani, katika hali ya kawaida imewezekanaje mtu kupatikana na wizi huo lakini bado akaendelea kuwa katika ofisi ya umma na baadaye kupigiwa chapua la kuchaguliwa tena ili arudi katika nafasi ile ile aliyotumia kuiba mwanzoni?
Hivi sisi Watanzania hatuwezi kuona, kuhisi, kusikia wala kunusa!
Pengine tuseme hivi hatuwezi kuona haya yanayotendeka wazi wazi. Mtu anakuibia halafu baadaye anaomba umchague tena arudi madarakani kwa kukuletea komedi ili usahau lile alofanya mwanzo. Je, sisi Watanzania ni watu wa aina hiyo?
Ndugu zanguni, bila kuwa wanafiki mnajisikiaje pale familia moja inapotumia jasho la mlipa kodi ili kufanya mambo ya kifamilia yasiyo ya msingi kwa ustawi wa taifa letu. Mume ndege, mke ndege, watoto magari ya bei kali. Hizi ni mali za nani hasa.
Watanzania, kwa pamoja tuinuke tukapige kura ili tuwatose hao wasiotufaa.
Tuanze na kuona mali zetu zinavyoliwa na watu wachache wasio na uchungu na nchi yetu.
Mambo ya msingi yanayotakiwa yafanyike ili sisi tujikomboe na umaskini tulio nao ni kuwekenza katika elimu. Hii ina maana elimu ni ufunguo wa maisha. Mtu aliyeenda shule akasoma na kuelewa anaweza kupata chakula bora, malazi na mavazi safi. Kwa maana hiyo kama elimu ndio msingi wa maisha kila mtoto wa Mtanzania anatakiwa apewe elimu bora. Ili kuweza kutimiza hili utoaji elimu hautakiwi kuwa na vikwazo vingi tunavyoona sasa. wengi ni mashahidi wa ukweli kwamba watoto wa walala hoi wameishia darasa la saba si kwa sababu hawana uwezo wa kuendelea juu hapana ila ni kwa sababu ya kutokupata fursa ya kusoma kwa kuwa wazazi wao hakuweza kuwalipia ada na michango mingine. Hii ina maana uwezo wa kifedha ndo kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya elimu nchini kwetu. Je, nani atbisha hilo? Kama tunakubaliana hapo, basi kwetu kiongozi anayetangaza elimu bure ndiye huyo anayetufaa sisi na si mwingine.
Kama nyumba ni sehemu ya mahitaji muhimu ya binadamu, ni kiongozi gani atakayetuwezesha sisi tujenge nyumba tuishi ili tuwe tumepata hitaji hilo la binadamu? Mimi nafikiri ni yule anayekumbuka hata kutuambia tu kwamba ujenzi wa nyumba utawezekana kama vifaa vya ujenzi vitakuwa vya bei ya chini ili wengi wetu tununue na tujenge nyumba. Kuongelea tu ujenzi wa barabara haitoshi maana barabara zinakumbukwa zaidi kwa kuwa hao wanaoiba na kufaidika kibinafsi na mali za nchi yetu ndo wenye magari ya kupitisha hizo barabara. Mimi mlala hoi cha msingi nyumba, elimu, na chakula. Barabara sawa lakini twende kwa vipau mbele ili kinachofanyika kimguse mwananchi wa chini kabisa.
Ili wananchi tuwe na nguvu ya kuleta serikali tunayotaka madarakani tunayo silaha moja kubwa: "KUPIGA KURA". Tusidanganywe ili tupige kura kumpigia mtu eti aliyetoa t-shirt, kofia na mabango. Mabango hayo ni fedha yetu inayotumika vibaya. Tunasema inatumika vibaya maana tungeondoa ubinafsi hiyo fedha iliyotumika kutengeneza mabango ingetununulia vitabu ili tusome tupate elimu bora.
Kwa kweli amini msiamini ndugu zangu, Tanzania yetu kwa sasa inahitaji matengenezo makubwa la sivyo huko tunako enda siko tuliko kusudia kwenda.

Thursday, October 21, 2010

TUACHE MAWAZO MGANDO

    Ndugu Watanzania wenzangu mnaoipenda nchi yetu, naomba wote kwa pamoja tufunge mikanda kuelimisha watu fulani ambao inaonekana mawazo yao ni ya zamani sana na inaonekana elimu waliyoipata waliipata kwa njia moja inayoitwa "indoctrination". Katika njia hii ya kupata uelewa fulani, mtu hupewa na kuaminishwa kitu fulani ambacho hicho atakisimamia mpaka hata afe lakini haachani nacho hata kidogo. Mtu huyo akiulizwa aeleze sababu za kung'ang'ana na hicho kitu mara nyingi haelezi vilivyo ila huishia kutetea na pengine ugomvi na yeyote anayekuwa tofauti naye katika mawazo.
    Jamani hivi inahitaji madarasa mangapi kuelewa kuwa duniani hapa wati hawafanani kwa sura na hata kwa mawazo? Inahitaji nini kujua kuwa kila binadamu hapa duniani ana kasoro zake ingawaje kuna tofauti katika uwingi wa kasoro kati ya mtu na mtu?
    Haya jamani. Jana magazeti yameandika kuwa Serikali inayatishia magazeti ya mwana Halisi na Mwananchi kuwa yatafungiwa sababu eti yanaichonganisha serikali na wananchi wake. AJABU! Hivi kusema kinyume na ulichopenda waseme ni uchonganishi? Kwa kweli ni ajabu kidogo. Ukiwa mtaani na ukakuta watu wamekaa wanaongea, utaona kuwa kila mtu anakuwa na wazo lake huyu hivi na yule vile. Sawa kwa kuwa hatufani!
     Magazeti hayo yaliyotajwa hayachonganishi ila nahisi mara nyingi yanaandika kile ambacho wakubwa wengi hawapendi kiandikwe. Hawapendi kiandikwe kwa kuwa hawajafanya kazi waliyotumwa na wananchi wakafanye. Wafikiria: Mbona magazeti haya yanaanika uovu wetu, tufanye nini kuyazima. Kama kweli magazeti haya yanaichonganisha serikali na wananchi ni habari ipi wameisema imechonganisha!!
Nawashauri serikali ifanye kile walichotumwa na wananchi waone magazeti yataandika nini. Hivi kama serikali imejenga daraja na inatoa elimu bure kwa wananchi na inashughulikia mafisadi ipasavyo kwa nguvu zote, itawezekana magazeti hayo kuandika kinyume na hapo kweli wakati matunda yanaonekana na wananchi wenye!HAPANA.
      Ili tuweze kumudu haya yote tunahitaji serikali safi. Usipokuwa msafi kila unakopita, kila unachosikia unalalama na kulalamika tu eti wananisema! TUAMKE.
      Pia kuna Watanzania mmoja mmoja wananichekesha sana. Hivi eti nyie watu hamuelewei kuwa mwalimu Nyerere naye alikuwa binadamu na kile alichoamini na kupigania si wote walikipokea? Kuna mtuwa ajabu na ajabu kweli na amenishangaza na kweli. Nasema amenishangaza kwa kuwa inaonekana ameenda shule lakini bado anaamini kuwa mtu yeyote aliyetofautiana na mwalimu Nyerere alau katika mfumo wa ujenzi wa taifa letu ni mdhambi kabisa na si tu wa kumfuata. Huyu jamaa amesoma lakini kichwani ana mawazo ya mgando kabisa.
   Mwalimu Nyerere, baba wa taifa letu, alifanya kazi kubwa sana kuikomboa tanganyika yetu toka kwa mkoloni na akatafuta mwelekeo wa taifa letu katika kukunza uchumi. Alijaribu na akafanikiwa kiasi fulani lakini pia yeye kama binadamu alishindwa hapa na pale na hili yeye mwenyewe anakiri hivyo.
   Kwa kuwa hakuwa malaika, kuna watu pia walioona mwelekeo aliochukua ulikuwa hauwaridhishi na hivyo hawakuwa pamoja naye kwa kila kitu kwa maana ya kuwa walikubaliana katika hili na wakatofautiana katika lile. Nani alikuwa sahihi, hilo hatujui!!
Tofauti hiyo haikumanisha kuwa watu waliotofautiana na mwalimu hawakuwa wazalendo, HAPANA. Walikuwa wazalendo tena wazuri kabisa na ndio maana wakajipambanua wakaonekana wametofautiana naye. Hivyo kwa mtu yeyote anayefikiri kutofautiana na mwalmu ilikuwa dhambi ana mawazo yaliyoganda kabisa.
     Huyu ndugu yetu Sheka ninamuomba atueleze zaidi kwa uwazi anachoona Mtei alikosa sana kwa kutokuwa pamoja na mwalimu katika mambo fulani kama kweli tofauti hiyo ilikuwepo. Je, babu yake Sheka hayupo katika historia ya ukombozi, hivyo tuseme hakuwa mzalendo? Hata kama Mtei hakushiriki kikamilifu katika mapambano ya kuikomboa Tanzania, kama ni kweli hivyo ndivyo, ni mawazo ya mbali sana kuona hilo linamwondolea haki ya kuanzisha chama. Kwani wote walowahi kushika madaraka walikuwepo wakati wa ukombozi miaka hiyo? SHEKA aachane na mawazo hayo. Labda kwa hayo aliyosema atuambie kwa uhakika masterpan ya CHADEMA ambayo sisi hatuifahamu ili tufahamu tupime. Lakini kama ni hiyo stori aliyokopi na kupesti, haijafanya chochote.http://www.mrmduda.blogspot.com
 

Saturday, October 16, 2010

HAKI NA AMANI


HAKI NA AMANI
  Haki na amani kwa namna moja au nyingine huitwa maneno pacha ingawa kila neno linaweza kuwa na maana tofauti na jingine.
  Neno haki kwa tafsiri au maana ya kawaida ni stahiki ya mtu kwa maana ya kile mtu astahilicho mtu kwa minajili ya kuwa binadamu au vinginevyo kama ilivyoainishwa katika jamii husika.
  Hii ni kusema kwamba zipo haki kama vile za kisiasa, kiuchumi, kijamii na nyingine nyingi kuendana na jamii yenyewe inavyoweza kuainisha kulingana na mahitaji katika jamii hiyo husika.
  Haki ya mtu au watu ikipokonywa au kuminywa mara moja hujibainisha kwamba hapa kuna jamba ambalo limekwenda kinyume. Madhara ya hili huwa kubwa kuliko hata gharama ya kuandaa haki hiyo.
  Ni madhila ya Haki ndiyo yanayotupatia Amani, kwamba palipo na Haki pana Amani. Kwa mantiki hii Amani ni zao la Haki. Neno amani lina dhana pan asana kwani inatiririka kutoka kwa mtummoja mmoja , kundi dogo la watu hadi jamii zima kwa ujumla wake.
  Kwa upande mwingine tunaweza kusema Haki huzaa imani na Imani huzaa Amani. Watu waliotendewa Haki, wasio na hofu Haki zao kufinyangwa, huwa na imani thabiti dhidi ya mamlaka zinazokabidhiwa jukumu la kutoa Haki hiyo.
  Hapa ndipo tunapoona upacha kati ya Haki na Amani, kwamba jamii iliyo na uhakika wa kupatiwa Haki zake itakuwa na Amani, na palipo na Amani ndipo maendeleo huwepo!
 Swali la kujiuliza hapa ni: je, jamii zetu zinapata Haki zake kwa kadri ya mahitaji yao? Amani ipo? Na kama ipo ni kwa kiwango gani? Kama haipo, ni kwa nini?
  Na je, kama wana jamii tunacho chochote cha kuchangia ili Haki na Amani viwepo? Tunashiriki vipi katika upatikanaji wake pasipo jamii kuparaganyika?
  Maswali yote haya na mengine mengi yanahitaji mjadala mpana kwa kila aliyepewa pumzi ya uhai na Mwanyezi Mungu kwa karama zake, wawe ni: wananzuoni au wanagenzi au wakurugenzi.
  Pengine kutokana na uzito na upana wa mjadala huu, ningependa niseme kila mmoja wetu ahusike ili tuweze kujifunza kwa pamoja na tuone jamii yetu inakwenda wapi na ipo katika hali ipi.
  Upo usemi usemao Haki yako inapoishia ndipo haki ya mwenzi inapoanzia
  Tujue kwamba kukosekana kwa Haki kumechangia sana kuongezeka kwa umaskini nchini mwetu.
  Fikiri kwa mfano, mwanafunzi wa elimu ya juu anahitaji mkopo. Katika fomu anayojanza, anatkiwa kugongewa mhuri mahakani.
  Anapofika mahakani anamkuta karani na kuambiwa kuwa inatakiwa igongwe mihuri sita na kila mhuri ni Tsh 1500. Huyu mwanafunzi anagongewa na hapewe risiti kuonyesha hiyo fedha inaingia kwenye mfuko wa nani.
  Au pia huyo mwanafunzi anashindwa kupata hiyo fedha na anaondoka. Na hivyo anaendelea kuhangaika maana bodi ya mikopo haitoi fedha kwa kuwa mwanafunzi huyo hakufanikiwa kigonga mhuri katika fomu huko mahakani. Je, huyu atakuwa na amani?
  Hivi ni nani alitakiwa ahakikishe kule mahakamani mambo yanaenda sawa. Siyo serkali yetu?
  Kwa kweli ndugu zangu pasipo na haki hakuna maendeleo yatakuwepo.
  Rushwa ikitawala, hakuna raia atapata haki yake. Hakuna mtu atakuwa na imani na mtawala wake.
Kinachohitajika hapa ni mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa masuala ya umma. Kama kuna wakati mtu aliyeonwa na kashfa ya kuchukua rushwa anataka tena achaguliwe awe kiongozi, na anachaguliwa, hivi kweli watu wa jamii hiyo wataonekana makini katika mamabo yao au wanafanya mchezo!!
  Hapa ndipo mgogoro wa upatikanaji wa haki na Amani katika jamii zetu unapoanzia: kwamba waliokabidhiwa keki ya taifa ili waigawe kwa Haki, humegeanamegeana. Sehemu kubwa ya keki hiyo huichukua wao wenyewe kwa manufaa yao na familia zao.
  Nimalinze kwa kusema Haki na Amani si swala la utashi, ni la lazima ili tuweze kupata ustawi wa kweli wa jamii zetu ili kutimiza usemi usemao: “Dunia unaweza kuitafsiri utakavyo wewe, lakini kinachotakiwa ni maendeleo”.

Friday, October 1, 2010

HUDUMA YA ELIMU, AFYA KUTOLEWA BURE INAWEZEKANA

Watanzania tusidanganyike kuambiwa kupata huduma ya afya na elimu haiwezekani!
Watu wengi wanaotafuta nafasi mbalimbali kutuongoza katika taifa letu la Tanzania wanatuambia kuwa huduma hizo zinaweza kutolewa bure.
Watu wengine wanapinga sana hoja hizo. Mimi nasikitika kuona kuna watu wanapinga wakisema huduma hizo haziwezi kutolewa bure!
Kadri yangu mimi nahisi inawezekana.
Kwanza, wakati wa mwalimu Nyerere miaka hiyo vitu hivyo vilitolewa bure kabisa. Kama katika kipindi hicho mambo hayo yaliwezekana iweje leo isiwezekane. Watuambia kitu ambacho kinafanya huduma hizo ziweze kutolewa bure.
Pili, wakati wa mwalimu Nyerere hapakuwa na miradi mingi kiasi cha miradi iliyopo sasa. Kadri ya wenyewe wanasema uchumi umekua. Kama uchumi umekua ina maana sasa tunao uwezo zaidi kuliko wakati huo. Kama tunao uwezo wa kiuchumi zaidi kuliko wakati huo, basi tunao uwezo zaidi wa kutoa huduma bure kuliko wakati ule.
Tatu, ufisadi mkubwa uliotokea katika nchi yetu unaashiria kwamba mali nyingi sana za nchi yetu zimefanya watu wengi tuamini kuwa kama pangekuwa na uaminifu katika serikali na ulinzi mahsusi wa mali za umma, basi watanzania wengi wangeamini kuwa huduma nyingi zaidi zenyi ubora zaidi zingewafikia Watanzania wengi zaidi.
Nne, misamaha ya kodi kwa wafanya biashara wakubwa inaonesha kuwa serikali haikusanyi mapato kwa makini zaidi ili kuhakikisha ina boresha huduma za jamii na pengine kuleta uwezekano wa kutoA HUDUMA HIZO BURE!
Tano, uzembe katika uimarishaji wa miundo mbinu yetu kwa ajili ya kukuza biashara zetu na nchi jirani unafanya watu waone kutoa huduma hizi bure haziwezekni! Kama tungeimarisha biashara yetu ya nje pato letu la taifa lingeongezeka sana na hivyo kuifanya serikali yetu iwe na uwezo wa kutoa huduma za kijamii bure.
Ukiangalia kwa makini sana utaona kuwa kutokuweza kufanya hivyo kunategemea sana watendaji wa serikali yetu waliopo madarakani. Kama wangejitoa kwa moyo wote kuwatumia wananchi mambo hayo yangewezekana.
Ili kuhakikisha tunakuwa na uwezo wa kupata huduma hizo za msingi bure, hatuna budi tudhamirie kweli tarehe 31-10-2010 tukapige kura na kuchagua viongozi wenye uwezo na mwelekeo chanya wa kuwatumikia wananchi kwa kuachana na viongozi mafisadi, wasio na uwezo wa kuona mbali na wenye ubinafsi ili wote na vizazi vyetu baadaye tufaidi matunda ya nchi yetu.