image slider

HUDUMA TUNAZOZITOA
Watengenezaji wa mashine za kuangulia vifaranga vya kuku
Wauzaji wa vifaranga vya kuku
Ushauri wa ufugaji wa kuku
Mashine za kuangulia vifaranga vya kuku
Wauzaji wa vifaranga vya kuku
Mashine za kuangulia vifaranga vya kuku

Tuesday, June 17, 2008

WAHEHE

Ungazija wa Wanyalukolo
na Mduda Expedito
KARIBU msomaji kwa mara nyingine tena katika safu yetu ya Ndivyo Ilivyo. Wiki iliyopita tuliitambua asili ya Wahehe wenye mchanganyiko wa Uhabeshi na niliwaahidi kumalizia simulizi zao kwa kuchunguza mchanganyiko wao na kizazi cha Kingazija.
Tukiendelea na baadhi ya makundi ya Wanitole ‘Wahabeshi’ ya Wahehe, ambayo sikuyataja wiki iliyopita, ni pamoja na Vahafiwa walioishi sehemu za Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalangombe, Ibanangosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe, Welu na Isanzala. Mtawala wao alikuwa Mwalyelu aliyetawala Welu hadi Pawaga ‘Mavaga’ na Mwamwano Mwansige aliyetawala Wutinde.
Majina ya watu wa kundi hili yalitokana hasa na kufa kwao kwa wingi kwa njaa na maafa, hawa ni kina Mwamugovano, Mwamaliga, Mwamukemangwa na Mwamuhesa. Husalimiana ‘kamwene hafiwa’ au ‘kamwene muponela’ ila kina Mwachaula husalimiana ‘kamwene lugome’. Vanyatengeta ni kundi lililoshi maeneo ya Uzungwa, Kitelevasi na Lundamatwe.
Hawa walikuwa ni mafundi wa kufua chuma, walioishi kwenye milima yenye asili ya milipuko ili kutafuta mchanga wenye chuma, baadhi yao ni kina Mwachusi na Mwamuvange. Salamu yao ni ‘kamwene tegeta’ ila kina Kalinga husalimiana ‘kamwene higo’, wao hawali mbawala.
Vanyakilwa ni watu walitokea Kilwa na kuishi maeneo ya Mufindi, hawa ni kina Mwalwagi na Mwakihwele, salamu yao ni ‘kamwene kilwa’. Vasavila waliishi juu ya milima ya Welu sehemu za Makungu, Magubike na Matogalu, hawa ni kina Mwamfilinge na Mwakasike. Vadongwe ni kundi lililoishi pembezoni mwa vilima katika maeneo ya Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Wao ni mchanganyiko wa Wanitole na Wasungwa na salamu yao ni ‘kamwene huvi’. Baadhi yao ni kina Mwamuyovela, Mwamaluvanga na Mwamukakilwa. Makundi haya ya Wahehe yanadhihirisha kuwa, wao ni mchanganyiko wa vizazi vya watu wa jamii tofauti tofauti. Hebu tuone mathalan, jinsi damu ya Kingazija ilivyoingia kwa Wahehe na kuleta utawala wa Muyinga, kizazi cha kina Mkwavinyika (Mkwawa).
Wenyeji wa asili wa Iringa kabla ya Mwamuyinga kuingia na kuanza kutawala, ni Wasungwa, ukiwaacha Wanitole kwa mujibu wa historia halisi iliyovurugwa na tawala za vikundi vya hao Wanitole.
Wasungwa huishi katika safu ya milima ya Usungwa iliyopo mashariki ya mji wa Iringa. Mwamuyinga ambaye pia ana majina ya Mbunsungulu, Mwakilyemikongi, Muhumba, Mdagaluhando na Lwimato, yaliyotokana na taabu alizozipata kutoka Ukaguru hadi Mahenge, lakini jina lake halisi ni Hasani Yusufu, mjukuu wa Hasani Hasani, mtu aliyetokea Ungazija kupitia Ushelisheli hadi pwani ya Afrika ya Mashariki, akitafuta vipusa, pembe za ndovu na kufanya biashara ya utumwa kama ilivyokuwa kawaida ya Waarabu wengi wakati huo.
Alifika Kilwa Kisiwani na kushinda vita alivyopigana na kulowea huko kwa kuoa mwanamke wa Kiafrika aliyemzalia mtoto aitwaye Yusufu Hasani, aliyerithi usultani wake hapo baadaye na kumuoa mwanamke wa Kiafrika pia aliyekuwa binti Mulimba na kuzaa nae watoto wawili wa kiume, Hasani au ‘Mbunsungulu’ na Ahmad.
Yusuf Hasani aliondolewa mamlakani na kuuawa na Wareno waliokuwa wanapiga vita utumwa. Hasani ‘Mbunsungulu’ na nduguye Ahmad walikimbilia Mafia walikopendwa sana na wenyeji wa huko na walianza kutawala huko, ambako Mbunsungulu alioa.
Wakati mkewe akisubiri kujifungua, taarifa za Wareno kutaka kuwafuata na kuwaangamiza baada ya kugundua kuwa wako huko, ziliwafikia kupitia kwa mjomba wao, Malik Sud, aliyenusurika kwenye mapambano Kilwa Kisiwani. Kwa hiyo, iliwalazimu Mbunsungulu, Ahmad na mjomba wao kukimbilia Ukaguru karibu na Kilosa.
Kabla ya kuondoka, Mbunsungulu alimuusia mkewe kuwa mtoto akizaliwa aitwe Wakinakuonewa. Mbunsungulu alioa tena huko alikokimbilia na mkewe alimzalia watoto watatu, Ngulusavangi, Mufwimi na Ngwila.
Mama huyo alihama na kukimbia na watoto wake kutoka Ukaguru kuelekea Upogoroni, maeneo ya Ulanga huko Mahenge, baada ya Mbunsungulu, Ahmad na mjomba wao, kuvamiwa na Waarabu na kuuawa.
Vijana hao watatu wakaondokea kuwa wawindaji hodari sana huko walikokimbilia na walikuwa hawanywi maji ya mito, kila jioni walichimba visima. Ugomvi uliowatenganisha ulitokana na jambo hilo pamoja na kitendo cha Ngwila kutangulia kuoa kabla ya kaka zake Ngulusavangi na Mufwimi bila ya idhini yao.
Kuna habari nyingi za vijana hawa wote watatu, lakini tutajihusisha zaidi na Mufwimi ambaye uzao wake ndio ulimleta Muyinga.
Mufwimi aliendelea na uwindaji akiwa na wafuasi wake Mwilapwa, Mafumiko na Mabiki pamoja na mbwa wawili; Ludoviko na Muhepapakwima.
Alisafiri hadi Dabaga katika maeneo ya Ng’uluhe akifikia kwanza Ikombagulu alikowaacha wafuasi wake kwa muda na kuendelea mbele kuwinda katika eneo lililotawaliwa na Mwamududa. Huyu bwana alikuwa na uwezo wa kuua nyati hata kumi kwa siku, aliichoma nyama porini na kuipaka chumvi na kumtumia mtawala Mwamududa na kwa kuwa watu wa huko hawakuwa wanaijua chumvi bado, Mwamududa alipoipata nyama hiyo iliyotiwa chumvi aliiona tamu sana.
Chumvi ilimfanya Mufwimi apendwe na kupewa ruhusa ya kuwinda atakavyo na alipokaribishwa, aliomba mahala pa kulala akapewa nafasi nyumbani kwa mtawala Mwamududa. Huko alianza kufanya mapenzi ya siri na binti wa Mwamududa aliyekataa kuolewa na wanaume wengi waliojitokeza kumposa, hatimaye alimpa mimba. Alipoambiwa juu ya mimba hiyo na yule binti, aliagiza mtoto akizaliwa salama akiwa wa kiume aitwe Mwamuyinga na akiwa wa kike aitwe Semuyinga.
Mwiko wake asile funo, mnyama mdogo wa porini jamii ya mbuzi na nyakihuko, mnyama afananaye na panya. Pia asiokote kuni za mti uitwao munyatomaa na kukokea moto. Mufwimi alitoroka usiku kwa kuogopa kuuawa na Mwamududa ambaye kumbe alipopata taarifa za ujauzito wa binti yake, alifurahi sana kwa kujua kuwa sasa angeolewa kirahisi. Mufwimi hakuwarudia tena wale wafuasi wake bali aliendelea kuwinda hadi huko Itamba, Usungwa alikouawa na nyati.
Wafuasi wake walipomtafuta, walipata taarifa za kuuawa kwake huko Itamba, lakini pia walipewa taarifa ambazo Mufwimi aliwasimulia wakazi wa huko juu ya binti wa Mwamududa aliyemwacha na ujauzito wake.
Waliamua kwenda huko kwa kujifichaficha, lakini walipodhihirika, walikaribishwa vizuri na kupewa makazi na mtawala Mwamududa aliyefurahi kupata mjukuu. Huyu Mwamuyinga mtoto wa Mufwimi, chotara wa Kimanga aliyekuwa jasiri tangu ujanani, alimrithi babu yake na kuanza kutawala sehemu hiyo ya Ng’uluhe akiwa ‘Mutwa’ wa kwanza wa kabila lililotoka nje ya Tanganyika.
Ni kutokea kwa huyu Muyinga wa kwanza ndipo ulifuatia mfululizo wa vizazi kupitia kwa watoto waliozaliwa, ambapo Maliga alimzaa Mudegela aliyemzaa Kilonge aliyemzaa Ngawona Lupembe aliyeuawa na mdogo wake Munyigumba, ambaye alianza kuitanua himaya ya Uhehe baada ya kushika utawala mnamo mwaka 1870.
Huyu aliwashinda kivita wababe wa Kinitole na kuyaunganisha makabila ya Iringa, watu waliokuja kuitwa Wahehe na wakoloni hapo baadaye kutokana na mlio wao wa kivita wanapotupa mikuki kwa kusema he he he! wakiashiria hatari.
Kutoka Mutwa huyu ndipo alifuatia kutawala Mukwavinyika, mtoto wa pili wa Munyigumba, ambaye jina lake mtawala huyu liliwashinda wakoloni kulitamka na hivyo kufupisha kwa kutamka Mkwawa.
Mkwavinyika alianza kutawala akiwa na miaka 19 na aliyapiga vita makabila yote yaliyozunguka himaya yake na kuwashinda watu kama kina Chabuluma, Mtwa wa Wangoni na Merere, shemeji wa Mtwa wa Wasangu. Mukwavinyika alipigana pia na wakoloni wa Kijerumani.
Msomaji, simulizi hizi za Wahehe ni ndefu sana na zenye mambo mengi mno, ikiwemo kujipa majina ya kujitapa kulikofanywa kwa idhini ya Mutwa baada ya kutenda matendo makuu, ushujaa wa kutupa mikuki, uwezo wa mbio za kufukuza maadui, dawa za ushindi wa vita nakadhalika. Kwa sasa hapa panatosha kumalizia simulizi hizi za Wahehe.

3 comments:

Umoja wa Ukoo wa Kivenule - KAUKI said...

Ndugu Mduda, nashukuru sana kwa historia ya Wahehe, imeaindika vizuri na imesheheni mambo mazuri na ya kufurahisi. Maoni na yangu ni kuendelea kutuhabarisha kuhusiana na Wahehe. kwa mfano ningependa kujua vita vya wahehe baina yao wenyewe. Pia naomba kujua kuna unataarifa zozote kuhusiana akina Tagumtwa kwa sababu nilipata habari alipigana vita na akafia vitani, yaani vita za LIGALU na MIGOHA. Alikuwa na shabaha (KUVENULA), Kuua "AVENWE" "IVENULA" angaza adui kwa mikuki. Pia naomba unijulishe zaidi kuhusiana na historia za maeneo kama Magubike, Ulefi, Mlafu, Nzihi. pia suala zima la Wabena Manga, Ukoo wa akina Balama, Sekaboko, Kivenule. Pia kama kuna habari za Luhota. Kwa leo naomba niishie hapa, natanguliza shukrani zangu za dhati.

Unknown said...

Mwl. nashukuru sana kwa historia hii kwani sijawahi hatakusoma kwenye vitabu, mwalimu wewe unakipaji nashauri kama unaweza iweke kwenye kitabu naamini watu watahitaji sana, watoto wanazaliwa tusipowalithisha dhana hii hawatajua wametokea wapi. Lakini pia kama una muda nashauri uandike kama kamusi ya kihehe yenye maneno ya kihehe na kutafsiri kwa kiswahili kwani watoto wa sasa wa international schools hata hawjui hata lugha ya asili yao. pia hata histori hii waweza iandika kwa kilugha na kuiweka kwenye vitabu. ikikaa kwenye maandishi naamini kupotea si rahisi. Nakutkia kazi njema na hongera sana.

19don said...

kuna mtu mwingine ameandika historia ya mkwawa katika hali nyingine kabisa sasa nikiwa kama mhehe naanza kujiuliza hizi history mbona zina tofautiana, huyu anasema jina la mkwawa lilitolewa kwenye kikao cha machifu wa sagara uhehe na ugogo kilichofanyika mlali sehemu za dodoma na jina la mpwapwa ndipo lilipo anzia baada ya mkwawa kusimikwa uchifu wa kihehe akiwa mpwa wa munyigumba sasa ipi ni ipi?
GOD MWAKINGUNZA