Ndugu Watanzania wenzangu wapenda nchi yetu iliyotukuka!
Mungu wetu alipoiumba dunia hii alikusudia viumbe wake wote wafurahi bila kuoneana. Kwa kufuata msingi huu, katika katiba za makundi mbalimbali kuna maneno kama "BINADAMU WOTE NI SAWA".
Kutokana na ukweli huu, watu kwa kutumia akili zao kubwa wakatafuta mitindo mbalimbali ya namna ya kuweka serikali zao madarakani. Watu wengi kwa sasa wanapendelea mifumo ya kidemokrasia. Mfumo huu unapendwa zaidi kwa kuwa hushirikisha watu wote kwa namna moja au nyingine katika kutoa maamuzi yanahusu jamii hiyo.
Demokrasia maana yake "Utawala unaowekwa na watu". Hivyo ili nchi moja iitwe ni ya kidemokrasia, lazima serikali ya nchi hiyo iwe imewekwa na watu.
Ili kudumisha hali ya utengamano ambamo watu wanajisikia wamo katika nchi yao, lazima mambo mengi ya kijamii yafanywe kwa uwazi mkubwa na maamuzi yao yaheshimiwe sana.
Kutokana na ukweli huo, sisi Watanzania pia lazima tufuate utaratibu huu wa kidemokrasia ili tusiwe na manung'uniko katika nchi yetu sote. Pale panapotokea kundi moja dogo la watu waroho wa madaraka wanahodhi maamuzi ya watu na kufanya kila kitu kiwezekanacho kudidimiza matakwa ya watu wengine, basi nchi huishia katika vurugu kubwa sana ambayo kuizima huwa ni taabu kubwa sana.
Ndugu Watanzania, juzi tumekua na uchaguzi mkuu ambao ulitakiwa utupe madiwani, wabunge na rais tunayemtaka.
Kitu kinachosikitisha sana ni pale tunapoona kuna dalili za makusudi kabisa za kupotosha hali halisi ya matokeo ya uchaguzi huo.
Watu wanasema matokeo yanayotolewa si yale ambayo yapo kwenye vituo vya kupigia kura. YANABADILISHWA!! Hivi jamani mnataka watu watumie lugha ipi kupata haki yao?
Kama ni kweli matokeo hayo si yale yanayotakiwa yatolewe, kweli mimi binafsi kama Mtanzania wa nchi hii, naomba turudishe matokeo halisi ili sisi wapiga kura tujisikie tumesikilizwa na tujisikie tumo katika nchi yetu.
Ndugu zangu, uchaguzi ni gharama kubwa sana. Lakini kama baada ya uchaguzi anatangazwa yule aliyechaguliwa, uchaguzi huwa na maana sana na haijalishi gharama yake. Kama uchaguzi ni gelesha ili watu wapumbae na walio madarakani wabadilishe matokeo waonekane wao ndo wamechaguliwa wakati siyo, kweli inauma sana na kila mwenye uchungu na nchi hii anasikitika sana. "EE MUNGU WETU MBONA UMETUACHA?".
Enyi vingozi wa dini mnayaona haya? Enyi wazalendo wa nchi mnayaona haya? Mwalimu Nyerere tunaomba ufufuke uone yanayoendelea!!
Watu wachache wameiba mali ya taifa letu. Watu wanaliangamiza taifa hili, na bado wanang'ang'ania kubaki madarakani hata pale wapiga kura wanapowakataa. Tumesikia kuna wagombea wanaoshindwa wanadiriki hata kuhonga wale wanaoshinda watangaze wameshindwa! Hivi jamani sisi wenye ngozi nyeusi hata akili yetu ni nyeusi? Mambo tunayofanya si sahihi hata kidogo. Ni uonezi mkubwa.
Leo hii mimi nikipata ubalozi wa nyumba kumi basi na watoto wangu wote na mke wangu ni mabalozi. Nao wanaanza kutoa matamko ya kibalozi kwa wau wangu. Gharama za uendeshaji wa ubalozi wa nyumba kumi inaongezeka kwa kuwa ubalozi huu ni familia yote! Jamani tunaomba huruma sisi Watanzania wenzenu, mbona hivi jamani?
Kumwita mwenzako kokoto ati kwa sababu tu ameamua agombee nafasi ambayo wewe unagombea siyo sawa hata kidogo kwani si wewe tu una haki ya kufanya hivyo.
Kutumia mali za umma kuhadaa watu ambao bado elimu yao ndogo ili wakuchague badala ya kuunza sera ya namna utavyoleta unafuu wa maisha yao si sawa hata kidogo!
Eti nyie watu, mbona nashangaa sana! Unajisikia vipi unapolazimisha watu wakuchague au hata kuiba kura uonekane umeshinda wakati pengine hukushinda. KWANI TUNAPOSEMA SISI NI WAUMINI WA DINI FULANI HUWA HATUMAANISHI? Maana muumini wa kweli ni yule anayezingatia maagizo ya MWENYEZI MUNGU!
Ndugu zanguni, kwa kuwa hili si jambo la mchezo tuombe wenzetu wanaofikiri ndo wenye haki zaidi ya nchi hii waache mawazo hayo na watoe nafasi kwa wananchi waseme wanataka nini! Kama kweli kuna njama za kuiba kura njama hizo ziazhwe mara moja na kila mmoja apate kura halali alizopewa na wananchi.
MUNGU IBARIKI TANZANIA!!
BLOG YA UJASIRIAMALI:UFUGAJI WA KUKU: KWA MAHITAJI NA USHAURI WA UFUGAJI WA KUKU NA MASHINE ZA KUANGULIA VIFARANGA VYA KUKU TUWASILIANE KWA NAMBA 0753903809 AU 0655903809
No comments:
Post a Comment