Tuesday, February 26, 2013

Sifa za banda bora la Kuku


Ukiamua kufuga katika banda kwa njia mbili zilizoelezwa awali utatakiwa kujenga banda
lenye sifa zitakazokidhi mahitaji ya msingi ya kuku. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa
kama ifuatavyo:
Liwe jengo imara
• Pasiwe na sehemu zilizo wazi kwenye msingi na kati ya ukuta na paa.
• Banda lijengwe na vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili liwe na gharama
utakayoweza kumudu.
• Unaweza kutumia matofali ya udongo, udongo, miti, fito,n.k. Ukitumia fito au mabanzi
ondoa maganda ili kuthibiti mchwa.
• Jengo mara litazuia maadui kama panya, vicheche, paka, nyoka na wezi kuingia ndani
ya banda na kuwadhuru au kuwaiba kuku.
Liwe rahisi kusafisha
• Kuta na sakafu visiribwe zisiwe na nyufa ili kurahisisha kusafisha.
• Pia itadhibiti kusiwe na wadudu wa kujificha katika nyufa kama papasi, viroboto n.k.
• Sakafu ya banda lazima iwekewe matandazo kama pumba ya mpunga au maranda
ya mbao au mabaki ya mazao au nyasi kavu kutegemeana na kinachopatikana kwa
urahisi katika mazingira yako.
• Matandazo haya husaidia kunyonya unyevu unaotokana na kinyesi cha kuku au maji
yanayomwagika katika banda.
• Banda hubakia kavu bila kuwa na harufu mbaya na wadudu kama inzi hata vimelea
vya magonjwa hudhibitiwa.
Eneo la nje kuzunguka banda kuwe na usafi wa kudumu
Hali ya usafi nje ya banda itafanya wadudu kama siafu au mchwa na wanyama kama
panya na paka mwitu wakose maficho. Nje ya banda ndani ya uzio kuwe na miti midogo
na mimea mingine midogo kwa ajili ya kivuli.

No comments: